Faida za Kusoma Vitabu Kwenye Maisha, Ni watu wachache sana Tanzania ndiyo wanaopenda na wanafahamu umuhimu wa kusoma vitabu. Watu wengi hasa waafrika hawapendi kusoma vitabu.
Kuna maarifa mengi yaliyofichwa kwenye vitabu hii ndiyo sababu watu wengi waliofanikiwa husoma au hata kuandika vitabu.
Faida za Kusoma Vitabu Kwenye Maisha
Kusoma vitabu ni moja ya njia bora kabisa za kujifunza, kujielimisha, na kujikuza kifikra. Vitabu vina uwezo wa kubadilisha maisha ya mtu, kuimarisha uelewa wa dunia, na kukuza maarifa katika nyanja mbalimbali.
Hapa chini ni faida muhimu za kusoma vitabu kwenye maisha ya binadamu:
1. Kusoma Vitabu Huongezea Maarifa Mapya
Lengo kubwa linalowafanya waandishi wa vitabu kuandika vitabu ni kuweka maarifa yao kwenye maandishi.
Hivyo kwa kusoma vitabu unapata maarifa mbalimbali yaliyowekwa kwenye kitabu husika.
Hivi leo kuna vitabu vinavyohusu takriban kila kitu; kwa hiyo maarifa yoyote unayoyahitaji unaweza kuyapata kwenye vitabu.
2. Kusoma Vitabu Husaidia Kufikiri Kwa Kina
Kwa hakika vitabu huongeza sana uwezo wa kufikiri.
Unaposoma vitabu unafahamu mambo ambayo yatakufanya ufikiri zaidi mara nyingine kitabu kitakuacha na maswali ambayo yatakufanya utafakari kwa kina zaidi juu ya mambo mbalimbali.
3. Kusoma Vitabu Huongeza Uwezo wa Lugha
Mbinu moja wapo ya kuongeza uwezo wa lugha ni kusoma machapisho mbalimbali yaliyoandikwa kwa lugha unayotaka kujifunza.
Kwa kusoma vitabu utaongeza msamiati, utajifunza sarufi ya lugha au hata mbinu mbalimbali za matumizi ya lugha.
Unachotakiwa kuzingatia hapa ni kusoma vitabu bora mara nyingi kadri uwezavyo.
4. Kusoma Vitabu Huburudisha
Vitabu ni burudani ya kipekee na ya gharama rahisi unayoweza kutembea nayo mahali popote.
Viko vitabu mbalimbali tena vya bei rahisi ambavyo vinaweza kukuburudisha na kukufurahisha.
Vitabu hasa vile vya kifasihi ni burudani tosha ya aina yake.
Unaweza kusoma vitabu vilivyochapishwa au vitabu pepe kwa kutumia simu au kompyuta yako.
5. Kusoma Vitabu Hukupa Hamasa
Maisha yana changamoto mbalimbali; hivyo utahitaji kitu cha kukuhamasisha kutoka hatua moja hadi nyingine.
Kwa kusoma vitabu vya hamasa kuhusu maswala mbalimbali ya maisha utaweza kuhamasika zaidi.
Vipo vitabu vilivyoandikwa kukuhamasisha au vilivyo andika maelezo ya watu waliofanikiwa na jinsi walivyopita kutoka changamoto moja hadi nyingine.
6. Kusoma Vitabu Huokoa Pesa
Vitabu havihitaji umeme, mafuta au matengenezo ili kufanya kazi.
Baadhi ya vitabu vingine pia hufundisha mbinu mbalimbali za kuokoa pesa.
Hali kadhalika kusoma vitabu kutakuokolea pesa nyingi ambazo ungezitumia kwenye maswala kama vile starehe.
7. Kusoma Vita Husaidia Kutumia Muda Vizuri
Unapotumia muda wako kusoma vitabu, ni wazi kuwa hutopata muda wa kupoteza.
Kusoma vitabu kutakufanya utumie muda wako kuongeza maarifa yako zaidi.
8. Kusoma Vitabu Huongeza Uwezo wa Uandishi
Ni lazima ujifunze namna waandishi wengine wanavyopanga mawazo, wanavyotumia lugha pamoja na mbinu nyingine za kiuandishi.
Huwezi kuwa mwandishi bora kama husomi vitabu vya waandishi wengine bora.
9. Kusoma Vitabu Huboresha Afya
Vipo vitabu vingi vinavyotoa maarifa juu ya kuboresha afya yako.
Kwa kusoma vitabu hivi utapata maarifa juu ya mambo unayoweza kufanya ili afya yako iwe salama na bora zaidi.
10. Kusoma Vitabu Huwezesha Kujenga Hoja
Ni ukweli usiopingika kuwa Fran Lebowitz alifahamu wazi kuwa huwezi kuzungumza kabla ya kufikiri na huwezi kufikiri kabla ya kusoma.
Kusoma kunakupa uwezo wa kufikiri na kujenga hoja zenye nguvu.
Ikiwa unataka kuzungumza ili watu wakuamini, basi soma vitabu kila mara.
11. Kusoma Vitabu Huongeza kipato
Waandishi mbalimbali wa vitabu wamekuwa wakiwafundisha wasomaji wao njia za kuongeza kipato chao.
Vipo vitabu vinavyofundisha juu ya mikakati ya uwekezaji pamoja na mbinu mbalimbali za kuongeza kipato.
Ukitaka kuongeza kipato ni lazima uongeze pia kiwango chako cha kusoma vitabu.
12. Kusoma Vitabu Huongeza Ubunifu
Tofauti kubwa iliyopo kati ya kusoma vitabu na kuangalia televisheni ni juu ya kuongeza ubunifu wako pia Kadri unavyosoma vitabu, ndivyo unavyojifunza mambo mapya zaidi ambayo yatakufanya kuwa mbunifu.
Kwa kusoma vitabu pia unaweza kufahamu jinsi watu wengine walivyotumia ubunifu kutimiza malengo yao pamoja na kukabili changamoto mbalimbali.
13. Kusoma Vitabu Huondoa Msongo wa Mawazo
Kusoma vitabu hukufanya uondoke katika lindi kubwa la mawazo yanayokutesa na kukutafakarisha juu ya mambo mengine.
Waandishi wa vitabu hujenga mazingira ambayo msomaji hujihisi yumo ndani yake.
Hivyo kwa kusoma vitabu, utaliwazwa, utafarijiwa na hata kutiwa moyo huku ukihamishwa katika mawazo yanayokutesa
14. Kusoma Vitabu Husaidia Kuacha Tabia Mbaya
Kwa njia ya kusoma vitabu unaweza kujifunza mbinu mbalimbali za kuacha tabia kama vile ulevi, uvivu, uzinzi na sigara.
Pia kwa kusoma vitabu utatumia muda vyema na kukosa muda wa kutekeleza tabia mbaya.
15. Kusoma Vitabu Huongeza Uwezo wa Kumbukumbu
Kadri unavyosoma vitabu ndivyo unavyoongeza uwezo wako wa kumbukumbu.
Kwani kila mara unaongeza mambo mapya ambayo unatakiwa kuyakumbuka.