Klabu ya Yanga imetangaza rasmi kuwa sherehe za kilele cha Wiki ya Mwananchi 2025, maarufu kama Yanga Day, zitafanyika Ijumaa ya Septemba 12, 2025 katika dimba la Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Hafla hii kubwa itafanyika siku mbili tu baada ya Simba Day 2025, iliyopangwa kuchezwa Septemba 10, jambo linaloweka wazi ushindani wa jadi kati ya vigogo hawa wa soka nchini.
Sherehe ya Yanga Day Kufanyika Benjamin Mkapa 12 Septemba 2025
Utamaduni wa Wiki ya Mwananchi
Wiki ya Mwananchi almaharufu kama Yanga Day ni tamasha kubwa la kila mwaka ambalo Yanga SC hutumia kushirikiana na mashabiki wake, kuonyesha mafanikio, na kuandaa misimu mipya ya mashindano. Kwa mwaka 2025, sherehe hizi zinatarajiwa kuvunja rekodi kutokana na mafanikio makubwa ambayo klabu imepata msimu uliopita pamoja na maandalizi ya kisasa yanayoendelea.
Shughuli Kubwa Zilizopangwa Katika Wiki ya Mwananchi 2025
Kwa mujibu wa taarifa rasmi za Yanga SC, sherehe za mwaka huu zitajumuisha matukio makuu yafuatayo:
1. Utambulisho wa Wachezaji na Benchi la Ufundi
Wachezaji wote wapya na waliopo pamoja na benchi la ufundi la Yanga SC watatambulishwa rasmi kwa mashabiki. Hii itakuwa fursa ya kwanza kwa Wananchi kushuhudia kikosi kitakachoingia vitani katika mashindano ya NBC Premier League na CAF Champions League msimu ujao.
2. Kuonyesha Makombe Matano ya Msimu Uliopita
Yanga SC itawapa mashabiki wake nafasi ya kipekee kushuhudia makombe yote matano waliyovuna msimu uliopita. Hii ni ishara ya ubabe wa klabu na mafanikio makubwa waliyoandika katika historia ya soka la Tanzania.
3. Mchezo wa Kirafiki na Timu Kubwa
Kama ilivyo desturi ya sherehe hizi, Yanga SC itacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya timu kubwa. Mchezo huu unatarajiwa kuwa kivutio kikuu kwa mashabiki, ukitoa ladha ya ushindani na burudani kabla ya kuanza kwa msimu mpya.
4. Utambulisho wa Timu za Yanga Princess na Yanga Youth
Mbali na kikosi cha wakubwa, timu za vijana (Yanga Youth) na timu ya wanawake (Yanga Princess) pia zitapewa nafasi ya kutambulishwa. Hii inalenga kuonyesha maendeleo ya klabu katika kukuza vipaji na kuendeleza soka la wanawake nchini.
5. Mgeni Rasmi Rais Samia Suluhu Hassan
Sherehe za Wiki ya Mwananchi 2025 zinatarajiwa kuhudhuriwa na mgeni rasmi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Rais Samia anatarajiwa kushiriki kwenye tamasha la Simba Day tarehe 10 Septemba, na kisha kuhudhuria kilele cha Yanga Day Septemba 12, jambo linaloonyesha umuhimu wa sherehe hizi kwa taifa zima.
6. Burudani za Kipekee
Mbali na michezo ya soka, sherehe hizi zitapambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii wakubwa wa muziki nchini. Mashabiki watafurahia muziki, tamasha la kijamii, na shamrashamra zinazolenga kuifanya siku hii kuwa ya kipekee kwa kila Mwananchi.