Tabia za Watu Waliofanikiwa Katika Maisha
Ni dhahiri kuwa watu waliofanikiwa ni tofauti na watu wengine kutokana na yale wanayoyafanya au kutofanya.
1. Watu Waliofanikiwa Hawapuuzi Uwekaji wa Akiba
Katika maisha ya kiuchumi kuna vipindi viwili cha kwanza ni kipindi cha mavuno na kipindi cha ukame na ni watu wachache sana ndio wanaoweza kuishi katika vipindi hivi viwili bila shida.
Watu waliofanikiwa hawapuuzi swala la kuweka akiba hata kidogo, kwani wanafahamu kuna kipindi watahitaji akiba hizo ziwasaidie kuishi maisha yao ya kawaida bila tatizo.
Hivyo basi, unatakiwa kujifunza kuweka akiba ili uweze kuishi kipindi cha ukame bila shida.
2. Watu Waliofanikiwa Hawategemei Watu Wengine
Ni kweli kuwa duniani tumeumbwa kushirikiana na kutegemeana, lakini si kwa kila kitu ila Ni wazi kuwa, watu waliofanikiwa wanafahamu umuhimu wa kusimama wao kama wao na si kutegemea watu wengine kwa kila kitu.
Unapotegemea watu wengine kwa kila kitu ni wazi kuwa hutoweza kufikia malengo yako kwani si wote watakaokuunga mkono ipasavyo.
3. Watu Waliofanikiwa Hawaishi Kama Wasio na Chakufanya
Mara nyingi watu hupenda kujishughulisha pale wanapopangiwa majukumu au wanaposimamiwa na mtu mwingine.
Lakini hali ni tofauti kwa watu waliofanikiwa kwani wao hujipangia majukumu yao na kujisimamia wenyewe Mara nyingi utawaona watu waliofanikiwa wakiandika, wakisoma vitabu na makala mbalilimbali au wakisikiliza hotuba Ilimradi tu wawe na cha kufanya.
Jifunze kuwa mtu mwenye tija kwa kuishi maisha ya watu waliofanikiwa; usiishi kama huna kitu au kazi za kufanya.
4. Watu Waliofanikiwa Hawabaki Kwenye Makosa Yao
Ni kweli umefanya kosa fulani na pengine athari zake unaziona katika maisha yako.
Lakini hebu jifunze kutokana na makosa na si kubaki katika hali mbaya ya kosa ukijilaumu, ukilalamika na hata ukijihukumu.
Watu waliofanikiwa hutumia makosa kama shule ya kuwafundisha kufanya mambo bora zaidi mbeleni na si kubaki katika makosa yao.
5. Watu Waliofanikiwa Hawaruhusu Zamani Zao Ziwashikilie
Kama ilivyo katika hoja ya kutoruhusu kubaki kwenye makosa, ndivyo ilivyo pia katika kutoruhusu zamani yako kukushikilia.
Tambua ya kale yamepita, na hauwezi kuibadilisha jana ila unaweza kuibadilisha kesho.
Ulikuwa na msingi mbovu kiuchumi katika familia au hukusomeshwa vyema ni baadhi tu ya hali za zamani ambazo haupaswi kuziruhusu kukuathiri.
Watu waliofanikiwa wanafahamu wazi athari za kuruhusu zamani zao kuwashikilia, hivyo wao hufanya kila jitihada kujinasua.
6. Watu Waliofanikiwa Hawategemei Bahati
Ni wazi kuwa wapo watu waliofanikiwa kibahati tu katika maisha, lakini hili si jambo la kutegemewa.
Watu waliofanikiwa hawaishi maisha ya kusubiri kushinda Bingo au bahati nyingine ili wafaulu kimaisha au watimize ndoto zao.
Watu hawa hufanya kazi kwa bidii wakijua kuwa katika juhudi ndiko hutoka mafanikio.
Hivyo nakuhamasisha kuacha fikra finyu za kungoja “dili” au “jiwe” ili ufanikiwe.
7. Watu Waliofanikiwa Hawapuuzi Mambo Ya muhimu
Nimeshuhudia wafanyabiashara wengi wa Kiafrika wakibweteka na kupuuza mambo ya msingi kwenye biashara zao.
Maswala kama vile kujali wateja, kutunza taarifa za kibiashara au kuboresha huduma. ni mambo ambayo watu waliofanikiwa huyapa kipaumbele.
Hivyo ni vyema ukajifunza kutokupuuza mambo ya msingi katika kazi au biashara yako.
8. Watu Waliofanikiwa Hawaogopi Kusema Hapana
Watu waliofanikiwa wanajua nguvu iliyoko katika jibu la “Hapana”.
Je, wajua kuwa hapana ni jibu rahisi au dogo sana lakini lina nguvu kubwa? Usikubali kuwa mtu anayepokea na kukubaliana na kila kitu.
Kwa mfano twende sokoni, unaenda; twende disko, unaenda; kunywa pombe, unakunywa; nakupenda, unakubali; twende tukatembee unaenda au vuta bangi na wewe unavuta.
Jifunze kusema hapana hata kama hutamfurahisha unayempa jibu hilo pia Watu waliofanikiwa wanajua kuwa jibu la hapana litawatenga na watu na mipango isiyo sahihi kwenye maisha yao.
9. Watu Waliofanikiwa Hawaachi Mawazo Yao
Mara nyingi tunapokuwa na wazo au mpango si rahisi kukubaliwa na kila mtu.
Wengine watakupinga kwa ajili ya wivu, chuki au kutokana na uwezo wao mdogo wa kufikiri.
Kwa kulifahamu hili watu waliofanikiwa hawaachi mawazo yao kwa kuwa tu yamepingwa na watu wengine.
Wao huyafanyia kazi mawazo yao kwa kutazama malengo yao na hatimaye hufanikiwa.
10. Watu Waliofanikiwa Hawapuuzi Vifaa Vyao vya Kielektroniki
Hivi leo watu wengi wanamiliki simu za kisasa au kompyuta.
Vifaa hivi vina matumizi mbalimbali, yenye tija na na yasiyo na tija.
Watu waliofanikiwa hawaachi kutumia vifaa vyao katika mambo yenye manufaa kwao.
Watu hawa huvitumia kujifunza, kufanya kazi mtandaoni na hata kuwasiliana kwa maswala ya msingi.
Kwa hiyo hata wewe unaweza kutopuuzia manufaa yaliyoko katika vifaa vyako vya kielektroniki kama ilivyo kwa watu waliofanikiwa.
11. Watu Waliofanikiwa Hawatengenezi Maadui
Watu waliofanikiwa wanajua si wote hupenda mafanikio; wengine hujenga uadui ili kukurudisha nyuma Mara nyingi maadui hujitokeza katika maisha, hasa pale unapofanya mambo ya maendeleo yenye kukinzana nao.
Lakini kuna maadui ambao unaweza kuwazuia; jitaidi kuondoka au kuachana na wale watu wanaotaka kutengeneza shari bila sababu.
Pia unaweza kubadili jambo au kuliacha kwa muda ili kuepuka kutengeneza maadui wasiokuwa na ulazima.
Zingatia pia kusamehe na kuwafanyia mambo mema wale waliokufanyia mabaya.
12. Watu Waliofanikiwa Hawajikwezi
Unyenyekevu na hekima ni karama adimu hasa kwa watu wanaoibukia katika mafanikio.
Lakini watu waliofanikiwa wanajua umuhimu wa kunyenyekea na kutojikweza.
Unyenyekevu hukupa nafasi ya kufanya bidii zaidi kwani hujioni kuwa umefika.
Pia unyenyekevu hukuweka karibu na watu wote; kwani hutomdharau au kumpuuza mtu yeyote.
13. Watu Waliofanikiwa Hawategemei Kitu Kimoja
Kuna usemi usemao “usiweke mayai yote kwenye kikapu kimoja” usemi huu unafahamika vyema sana na watu waliofanikiwa.
Watu waliofanikiwa huwa hawategemei kitu kimoja pekee; yaani kitu kimoja kikishindwa wao nao wameshindwa.
Jifunze kuwekeza katika mambo mbalimbali ili moja likikwama basi lingine liendelee.
14. Watu Waliofanikiwa Wanajua Kuwa Mambo ni Rahisi
Safari ya mafanikio ina milima na mabonde na Kujidanganya kuwa mambo ni rahisi na hakuna changamoto zozote ni tatizo kubwa.
Watu waliofanikiwa wanajua mambo siyo rahisi, wanafahamu kuwa watakutana na changamoto hivyo hujiandaa kuyakabili.
15. Watu Waliofanikiwa Hawatengenezi Hatari Bila Sababu
Inawezekana una fedha fulani za ziada, kila unachosikia na kuona unataka kuweka pesa zako. Huku ni kujitengenezea hatari zisizokuwa na sababu.
Siyo muhimu pia, kuhusiana na kila mtu kwani siyo wote wanakufaa; wengine ni kujitengenezea hatari au madhara yasiyokuwa ya lazima.
Jambo hili linafahamika vyema kwa watu waliofanikiwa hivyo hawajitengenezei hatari zisizokuwa za ulazima ili kuhakikisha kuwa wanafikia malengo yao.